Mashambulio ya anga yalioendeshwa na majeshi ya Urusi leo, yameua takribani watu 9 na wengine kujeruhiwa leo jumapili March 13, 2022, ambapo imeharibu vibaya kambi ya jeshi ya Yuvoriv nje kidogo ya Mji wa Lviv, jirani na mpaka wa nchi ya Poland.
Gavana wa Mji wa Lviv amesema huenda idadi ya waliokufa ikaongezeka ambapo mpaka sasa idadi ya majeruhi imefikia 57, wengi wakiwa na hali mbaya ambapo magari ya kubebea wagonjwa yameonekana yakiingia na kutoka kwa wingi katika eneo la tukio.
Shambulio hilo lililojumuisha takribani makombora tisa yaliyopiga kwa mfululizo kutokea angani, linatajwa kuwa baya zaidi katika siku za hivi karibuni na la kwanza kutokea upande wa Magharibi mwa Ukraine jirani na mpaka kati ya nchi hiyo na Poland.
“Wameshambulia katika kituo cha kimataifa cha kulinda amani na kambi yetu ya jeshi,” amenukuliwa Maxim Kozitsky kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Facebook.
Kambi hiyo iliyopo kilometa 25 kutoka katika mpaka wa Ukraine na Poland, inatajwa kuwa ndiyo kambi kubwa zaidi ya kijeshi Magharibi mwa nchi hiyo ambako mafunzo ya mara kwa mara ya jeshi la Ukraine yalikuwa yakifanyika kabla ya uvamizi wa majeshi ya Urusi.
Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Oleksii Reznikov amesema wakufunzi wa kijeshi kutoka nchi marafiki, huendesha mafunzo ya kijeshi kwa wanajeshi wa Ukraine katika kambi hiyo ingawa amesema hawana taarifa kamili kama walikuwepo eneo la tukio wakati shambulizi hilo likitokea.
Mji wa Lviv umekuwa ukitumiwa na wakimbizi wengi wa Ukraine wanaokimbia mapigano wakiwa wanaelekea kutafuta hifadhi katika nchi jirani ya Poland.
Wakati huohuo, Meya wa Lviv, Ivano-Frankivsk amesema mashambulizi mengine yameulenga uwanja wa ndege wa Lviv asubuhi ya leo, Jumapili.
Kwa upande mwingine, ving’ora vinavyoashiria mashambulizi ya anga yanakaribia kutokea, vimesikika asubuhi ya leo, Jumapili katika Mji Mkuu wa Kyiv ambapo Rais Volodymyr Zelenskyy ameyaonya majeshi ya Urusi kwamba yatapata madhara makubwa endapo yataendelea na majaribio yake ya kuuteka Mji wa Kyiv.
Rais Zelensky amesikika akisema miji mingi midogo imeharibiwa vibaya na mashambulizi ya anga ya Urusi na kueleza kwamba hayo ni mashambulizi makubwa zaidi tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Hapo jana, Ukraine iliishutumu Urusi kwa kuwashambulia na kuwaua raia saba wakiwemo wanawake na watoto waliokuwa wakijaribu kuukimbia Mji Mkuu wa Kyiv, madai ambayo Urusi imeyakanusha.