Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans umejizatiti vilivyo, ili kufanikisha kikosi chao kinapata ushindi kwenye mchezo wa Mzunguuko watano wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya US Monastir ya Tunisia.
Mchezo huo utashuhudia Young Africans ikicheza nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili (Machi 19) kwa mara ya pili mfululizo, baada ya kufanya hivyo dhidi ya AS Real Bamako ya Mali, iliyokubali kufungwa 2-0, Jumatano (Machi 09).
Mamaku wa Rais wa Young Africans Arafat Haji amewaambia mashabiki wa timu hiyo kuwa, uongozi wao umeanza mikakati ya ushindi katika mchezo wao dhidi ya US Monastir ya nchini Tunisia ambao wanauchukulia kama Fainali kwao.
Katika mchezo huo, kikosi cha Young Africans kitaingia uwanjani kikiwa na hasira za kufungwa Tunisia katika mchezo wa Mzunguuki wa kwanza ambao US Monastir walishinda mabao 2-0.
Akizungumza na Dar24 Media Arafat amesema bado hawajamaliza kazi, licha ya kuwafunga AS Real Bamako mabao 2-0 na TP Mazembe 3-1 kwenye Uwanja wa Mkapa, hivyo wana kibarua kigumu kuhakikisha wanafuzu Hatua ya Robo Fainali.
Arafat amesema kuwa bado safari yao hawajafika na mchezo dhidi ya US Monastir wanauchukulia kama Fainali, kwani lengo lao ni kulipa kisasi cha kufungwa ugenini mabao 2-0.
“Kwanza kabisa niwashukuru mashabiki wa Yanga, waliojitokeza kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa tulipocheza dhidi ya AS Real Bamako katika mchezo wa Jumatano.”
“Licha ya kushinda mchezo huo, lakini bado kazi hatujamalizika, tunahitaji kuweka mikakati kabambe ili kuhakikisha tunawafunga US Monastir Uwanja wa Mkapa, kwani huu ndio mchezo wa Fainali kwetu, ili kujihakikishia kucheza Robo Fainali.
“Kama uongozi wenu tunaingia msituni kuanzia sasa nanyi iwe hivyo kuanzia mchezo wa ligi, malengo yetu kutoacha alama yoyote nyumbani, sisi ndio Wananchi wenye ubora tutakaoendelea kuwa mfano wa kuchukua bonasi zote za Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema Arafat.
Young Africans ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Kundi D ikiwa na alama 07 baada ya kucheza michezo minne, ikitanguliwa na US Monastir ya Tunisia iliyojizolea alama 10 hadi sasa.
TP Mazembe inashika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 03, na AS Real Bamako inaburuza mkia wa Kundi hilo kwa kuwa na alama 02.