Serikali imewataka wananchi kujenga utamaduni wa kufanya usafi na kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku kwa kuhakikisha maeneo yao yanakuwa safi na salama kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi.
Hayo yamebainishwa jijini Dodoma na Waziri wa Kilimo, Antony Mavunde na kuongeza kuwa ni wajibu wa Wafanyabiashara kushirikiana na taasisi za Serikali katika kusimamia usitishaji wa Matumizi ya bidhaa za plastiki.
Awali, akimkaribisha Mgeni rasmi, Kaimu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Switbert Mkama alisema katika kukamilisha kilele cha maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani, Ofisi hiyo imejipanga kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma hatua inayolenga kupendezesha taswira ya Jiji hilo ambalo ni makao makuu ya Serikali.
alisema, “kuanzia jana (Juni Mosi, 2023), ambayo tulizindua Wiki ya Mazingira tumeanza kwa kufanya
usafi wa mazingira na kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma. Zoezi hili litaendelea hadi siku ya Kilele Siku ya Jumatatu Juni 5 mwaka huu.”
Akitoa salamu za Mkoa wa Dodoma, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Godwin Gondwe ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amesema Mkoa huo itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuhakikisha kuwa Jiji la Dodoma ambalo ni Makao Makuu ya Serikali linaendelea kuwa safi.
Kilele cha Wiki ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo ina kauli mbiu isemayo Pinga Uchafuzi wa Mazingira unaotokana na Taka za Plastiki inatarajia kuwa Juni 5 mwaka huu, ambapo Mgeni rasmi anatarajia kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango.