Uongozi wa Simba SC umeweka wazi kuwa hawatoshindwa kumsajili mchezaji yeyote watakayemtaka kulingana na thamani yake kutokana uwepo wa mwekezaji na Rais wa Heshima wa klabu hiyo, Mohammed Dewji ‘Mo’.
Simba SC imetoa kauli hiyo baada ya taarifa kuwa wameshindwa kupata saini ya beki wa Cameroon, Che Fondoh Malone ikidaiwa kuwa anatakiwa na klabu mmoja nchini Zurich.
Hivi karibuni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, alikutana na uongozi wa Coton Sport ya Cameroon juma lililopita kwa ajili ya majadiliano ya kupata saini ya nyota huyo ambaye muda wowote atasaini mkataba wa miaka miwili kutumikia klabu hiyo ya Simba SC.
Meneja wa Habari na Mawasiliano ya timu hiyo, Ahmed Ally, amesema kuwa kama kuna taarifa ya mchezaji yeyote ambaye anatakiwa na Simba SC basi wanauwezo wa kumnunua kutokana na bajeti yao kubwa waliyoiweka kwa ajili ya msimu ujao.
“Kama kweli huyo beki anatakiwa au mchezaji yeyote basi Simba SC haishindwi kumnunua, timu inayomilikiwa na Mo Dewji hatushindwi kumpata, hatusajili wachezaji waliokuwa huru bali tunaenda kuwanunua kutoka ndani ya klabu husika.
“Mapendekezo ya usajili ni kupata beki kuja kusaidiana na Joash Onyango na Henock Inonga kwa msimu ujao wa mashindano, lazima tufanye usajili bora kulingana na mahitaji yetu na mashindano tunayoenda kushiriki,” amesema Ally.