Kiungo Mshambuliaji wa Azam FC, Idd Seleman ‘Nado’ amekitazama kikosi cha timu yake hasa wachezaji anaocheza nao nafasi moja, ameona kuna kazi ya kufanya kuhakikisha kiwango chake kitamruhusu kucheza kikosi cha kwanza.
Nado ambaye msimu uliopita alimaliza na mabao saba, alikiri kuna ushindani, kila mchezaji anatamani kucheza kikosi cha kwanza, jambo linalomfanya akaze buti kwenye maandalizi ya msimu mpya ili kujiweka fiti.
Kwenye nafasi anayocheza, kuna wachezaji wenye viwango vikubwa kama Kipre Junior, Abdul Suleiman ‘Sopu’ Djibril Sillah ambaye ni mgeni ametokea Raja Club Athletic ya Morocco, Yahya Zayd, Ayoub Lyanga na Evans Tepsi ambaye hakuwa na nafasi kubwa msimu uliosha.
“Natamani kila msimu niwe na vitu vipya ambavyo vitamfanya kocha aone huduma yangu ni muhimu, mfano msimu ulioisha nilipania kufanya makubwa, lakini kuna wakati majeraha yaliniandama lakini nashukuru Mungu sikumaliza kinyonge nilifunga mabao saba.
“Kila idara ina mafundi, ili thamani yako ionekane kwenye klabu ni kufanya vitu vya ziada ambavyo kocha akivitazama anajua kabisa vinakuwa na faida, Ligi Kuu ijayo itakuwa ngumu sana.”
Mbali na hilo, Nado amesema kinachomsaidia asitoke nje ya kiwango chake ni kila msimu kujiona kama anakuwa na deni kwa klabu iliyomsajili kwa sababu inamlipa mshahara anaotakiwa kuutolea jasho.