JKT Tanzania imeendelea kujiimarisha ili kutisha Ligi Kuu Bara msimu ujao baada ya kupanda msimu huu ikitokea Championship, na sasa imenasa saini ya beki wa kulia George Aman Wawa kutoka Geita Gold ikimpa mkataba wa miaka miwili.
Wawa amekuwa mchezaji watatu JKT Tanzania kumchomoa Geita katika kipindi hiki baada ya hapo awali kuwanasa Danny Lyanga na Deusdedith Okoyo.
Taarifa zinasema kuwa JKT Tanzania imemnasa Wawa akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na matajiri wa dhabahu.
Sambamba na Wawa, Okoyo na Lyanga pia JKT imeshanasa saini ya Ismail Aziz Kader aliyetemwa na Azam na iko mbioni kukamilisha usajili wa kiungo wa zamani wa Simba na Mtibwa Sugar, Said Ndemla.
Kocha mkuu wa JKT Tanzania, Malale Hamsini amesema lazima aongeze wachezaji wapya kikosini ili kuendana na kasi ya Ligi Kuu.
“Tutafanya usajili mkubwa. Championship ni tofauti na Ligi Kuu, hivyo lazima tuwe na wachezaji wanaoweza kuendana na kasi ya ligi hiyo msimu ujao,” amesema Malale aliyeipandisha JKT Tanzania.