Mipango ya usajili wa kiungo kinda kutoka nchini Ufarsana Mattéo Guendouzi Olié ya kujiunga na klabu ya Arsenal, iliyokua ikifanywa siri imefichuliwa na kuwekwa hadharani.
Tovuti ya The Sun imefichua mipango hiyo kwa kuweka picha mnato na Video zilizoonyesha kinda huyo akisaini mkataba na mmoja wa viongozi wa klabu ya Arsenal hapo jana.
Kinda huyo mwenye umri wa miaka 19, ameonekana katika picha hizo akiwa katika kituo cha kufanyia mazoezi cha klabu ya Arsenal (London Colney).
Mkuu wa kitengo cha usajili na makubaliano wa Arsenal Huss Fahmy, alionekana katika picha hizo, akisimamia zoezi la kusainiwa kwa mkataba wa mchezaji huyo ambaye inadaiwa amejiunga na Arsenal kwa ada ya Pauni milioni 7 akitokea Lorient.
Taarifa zimeendelea kueleza kuwa, Guendouzi amesaini mkataba wa miaka mitano, ambao utamuweka Emirates Stadium hadi mwaka 2023.
Mchezaji huyo amekamilisha mpango wa kusajiliwa na Arsenal, akitanguliwa na kiungo mkabaji kutoka nchini Uruguay Lucas Torreira, ambaye jana jioni alitambulishwa rasmi, baada ya kukamilisha uhamisho wake akitokea Sampdoria ya Italia kwa ada ya Pauni milioni 22.