Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi – OSHA, kupitia Mtendaji Mkuu, Khadija Mwenda umesema kuwa wanafanya kazi kubwa kuhakikisha wanalinda Rasilimali Watu ambao ni uwekezaji wa Serikali Nchini.
Mwenda ameeleza kuwa, OSHA ni wakala wa Serikali iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu), ulianzishwa Agosti 31, 2001 kama sehemu ya mpango wa maboresho ya kutoa huduma kwa wananchi.
Hayo yameelezwa Desemba 7, 2023 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi cha Wanahabari kinachoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
“Serikali ilikaa ikaona hapana, lazima kuwe na chombo ambacho kama huyu mtu ataingia kwenye ajira lazima ijue anafanya kazi katika mazingira gani. Kikatengenezwa chombo kinachoitwa OSHA ili kisimamie mazingira ya kazi na kumlinda mfanyakazi.Tunafanya kaguzi ili kulinda uwekezaji wa rasilimali watu ambayo Serikali imewekeza,” amefafanua.
Katika kifungu Na. 16 cha Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, kinafafanua kuwa wamiliki au wasimamizi wa sehemu zote za kazi nchini wanapaswa kuhakikisha kwamba maeneo husika ya kazi yanasajiliwa na OSHA ili kuiwezesha taasisi kuwafikia kwa ajili ya kuwapa huduma nyinginezo za masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi.
Aidha, uchunguzi wa afya za wafanyakazi ambao hutekelezwa na wakaguzi wa afya wa OSHA hufanyika katika hatua tatu muhimu ambazo ni kabla ya kuanza kazi, mfanyakazi akiwa kazini na mfanyakazi anapoachana na mwajiri wake kwa sababu mbalimbali ikiwemo kustaafu, kuacha kazi, kuondolewa kazini, huku kukiwa na ongezeko la upimaji huo kwa asilimia 163 kutoka wafanyakazi 363,820 hadi wafanyakazi 955,959 waliopimwa katika kipindi kilichopita.
Katika hatua nyingine, Mwenda amesema OSHA imeondoa ada ya usajili wa eneo la kazi iliyokuwa ikitozwa kati ya shilingi 50,000 hadi shilingi milioni 1.8, ada ya fomu ya usajili sehemu za kazi shilingi 2,000; kufuta faini zinazohusiana na ukosefu wa vifaa vya kuzimia moto ya shilingi 500,000, ada ya leseni ya ithibati iliyokuwa inatozwa shilingi 200,000 kwa mwaka, pia wameondoa ada ya ushauri wa kitaalamu wa usalama na afya ya shilingi 450,000, ada ya mafunzo ya elimu kwa umma iliyokuwa inatozwa kiasi cha shilingi 250,000 kwa kila mshiriki; kupunguza ada ya uchunguzi wa ajali iliyokuwa ikitozwa shilingi 500,000 mpaka shilingi 120,000.
Pia wameondoa ada ya kipimo cha mzio iliyokuwa ikitozwa shilingi 25,000 kwa mfanyakazi, ada ya kipimo cha kilele cha upumuaji iliyokuwa shilingi 10,000 kwa mfanyakazi, ada ya huduma za ukaguzi wa mifumo ya umeme katika vituo vya mafuta vilivyopo vijijini kutoka shilingi 650,000 hadi shilingi 150,000 kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji katika maeneo hayo na kupunguza athari zinazoweza kutokea kutokana na utunzaji wa mafuta kwenye chupa za maji na madumu, suala ambalo linahatarisha maisha ya wananchi katika maeneo hayo. Pia wameondoa ada ya ukaguzi wa usimikaji wa pampu za gesi kwa kila kituo ambayo ilikuwa inatozwa shilingi 20,000 kwa kila pampu.
Ameainijsa mafanikio mengine ni usimikaji na Uboreshaji wa Mifumo ya TEHEMA, Kuimarisha Mifumo ya Usalama na Afya katika Miradi ya Kimkakati, Tanzania kutambulika Kimataifa katika Masuala ya Usalama, Afya Mahali pa Kazi na Ujumuishaji Sekta isiyo rasmi katika Mfumo Rasmi wa Usimamizi wa Maeneo ya Kazi na mengine mengi.