Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema ifikapo Desemba 2023, utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini wa awamu ya tatu mzunguko wa pili katika Vijiji vyote utakamilika na hivyo kupelekea kuanza utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme vitongojini.
Kapinga ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo Mkoani Tabora, ambapo katika siku ya pili ya ziara yake amewasha umeme katika kijiji cha Katunda kilichopo Wilayani Uyui.
Amesema,“tunatarajia kumaliza kazi ya kusambaza umeme vijijini ifikapo mwezi Desemba mwaka huu, nawahimiza wakandarasi fanyeni kazi yenu kwa uadilifu mkubwa, hatuhitaji kukimbizana juu ya hilo kila mmoja atekeleze jukumu lake kwa maslahi mapana ya taifa letu.”
Aidha, Kapinga amewaagiza wakandarasi wote nchini kuhakikisha kuwa vifaa vya kufanyia kazi vinakuwepo wakati wote katika maeneo ya miradi, ili kurahisisha utekelezaji wa mradi huo na hivyo kuukamilisha kwa wakati.