Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo amesema ushirikiano baina ya viongozi na watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais umechangia katika kudumisha Muungano na kuimarisha usimamizi endelevu wa mazingira.
Dkt. Jafo ametoa kauli hiyo wakati akifungua Kikao kazi cha Watumishi wa Ofisi hiyo kilichofanyika jijini Dodoma na kuwahimzia wasimamizi wa miradi inayotekelezwa na Ofisi hiyo kuendelea kuisimamia vyema ili iendelee kueleta tija kwa wananchi katika maeneo yenye changamoto za mazingira.
Aidha, ameshukuru na kuwapongeza viongozi na watumishi kwa ujumla kusukuma mbele ajenda ya mazingira kupitia usimamizi wa kanuni na miongozi mbalimbali ya mazingira akisema, “nitoe pongezi za dhati kwenu kwani mmetumia vyema utaalamu wenu katika kusimamia vizuri hifadhi ya mazingira kupitia kampeni zetu mbalimbali za mazingira.“
Hata hivyo, amewahimiza watumishi hao kuishi kwa kupendana na kutimiza wajibu wao kwa kufanya kazi kwa ufanisi na kwa kujituma, ili kuacha alama nzuri, huku akiwataka kutumia fursa ya teknolojia inayopatikana ili kuboresha mazingra ya kazi na hivyo kufanya utendaji wa kazi kuwa wenye tija.