Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amesema ushirikiano wa kisekta katika ufanyaji kazi ni jambo zuri linaloleta ufanisi na ubora katika kazi zinazokuza uchumi wa Taifa.
Dkt. Yonaz ameyasema hayo baada ya kutembelea na kukagua miradi ya kimkakati iliyoko visiwani Zanzibar, ukiwemo wa Bandari Jumuishi wa Manga Pwani, Nyumba za Makazi na Biashara pamoja na mradi wa nyumba za gharama nafuu.
Amesema, “Taasisi zetu zitaendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kutengeneza Uchumi imara katika eneo letu la Afrika Mashariki na Kati, na tukitambua kwamba soko letu linazidi kukua lakini sisi kama Nchi pia tuna fursa katika soko la SADEC, kwa hiyo tukizingatie tunapakana na nchi nyingi hivyo tukitumia vizuri tunayo nafasi ya kujenga uchumi.”
Aidha, Dkt. Yonazi ameongeza kuwa Serikali imefanya uamuzi kuanzisha kurugenzi za Ufuatiliaji na Tathmini katika kila Wizara ambapo itasaidia Serikali kufuatilia miradi yake ,mipango yake na kufaya maamuzi ya kiutendaji kwa wakati.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji Tume ya Mipango Zanzibar, Dkt. Rahma Salim Mahfoudh amesema jukumu la msingi la Ufuatiliaji na Tathmini Zanzibar ni kupanga na kufuatilia miradi ambapo kwa sasa wanampango wa muda wa kati wa mwaka 2021 na 2026.
“Tuna miradi ya Kimkakati ambayo tunapoifanya inaongeza ufanisi katika kazi yetu na katika Miradi mliyotembelea leo ni Miradi ya kimkakati ya Nchi ambayo tunawapa sapoti kwa asilimia mia moja hasa kwa mradi kama shirika la nyumba ni fedha za serikali ambazo zimeingizwa ili kuufanya mradi ule,” alisema Katibu Mtendaji.
Viongozi na Maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu wako visiwani Zanzibar kwa ziara ya siku mbili ya kujifunza utendaji kazi wa Idara ya Ufutiliaji na Tathmini ya Tume ya Mipango Zanzibar.