Jeshi la Polisi mkoani Tabora limewataka viongozi wa dini na wananchi kutoa ushirikiano ili kukabiliana na imani potofu za kishirikina zinazopelekea uwepo wa matukio ya mauaji.
Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi Mkoani Tabora, Barnabas Mwakalukwa wakati akizungumzia matukio ya ajali za barabarani kwa mkoa huo na kusisitiza suala la utii wa sheria bila shurti ili kuzuia matukio yanazoweza kuepukika.
“Watu wanauana eti kisa jirani yake amepata mazao mengi kuliko yeye hii yote inatokana na watu kukosa hofu ya Mungu wakati umefika na tuwaombe viongozi wa dini tushirikiane kutomeza tatizo hili,” amefafanua Mwakalukwa.
Kuhusu ajali za barabarani Mkoani Tabora Kamanda Mwakalukwa amesema zimepungua kwa asilimia 78 kutokana na juhudi za jeshi hilo kwa kushirikiana na wananchi, wadau na wasafirishaji ikiwemo kutoa elimu juu ya uzingatiaji wa sheria za usalama barabarani.
“Tumepunguza ajali kwa kiasi kikubwa na katika kipindi hiki cha sikukuu madereva wa vyombo vya moto na hata wale wa baiskeli ni vyema wakawa makini kwa kuzingatia alama za barabarani la sivyo watasherehekea siku kuu mahali pasipo faa,“ amesisitiza Kamanda Mwakalukwa.
Amesema mbali na masuala ya barabarani pia katika msimu huu wa sikukuu wananchi wanapaswa kuimarisha ulinzi na usalama wa mali zao ikiwemo kutoa taarifa kwa jeshi la polisi zitakazowezesha kukabiliana vitendo vya wizi na uvunjifu wa amani.
Akizungumzia kupungua kwa uhalifu katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo Kamanda Mwakalukwa amesema hali hiyo imefanikiwa kutokana na operesheni yao ya “FUKUAFUKUA” na kubainisha uwepo wa ongezeko la vitendo vya ulawiti.