Kampeni ya Uzalendo na Utaifa ‘Nchi Yangu Kwanza’ itazinduliwa Ijumaa hii Disemba 8, 2017 kupitia ‘Usiku Wa Kitendawili’ mjini Dodoma ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na msanii wa muziki wa asili nchini, Mrisho Mpoto kupitia Kikundi cha Sanaa cha Mpoto Theatre Gallery na wadau wa sanaa za Ubunifu ndio wataouratibu usiku huo wa Kitendawili.

Akizungumza na wadau wa sanaa katika Maandalizi ya Kampeni hiyo ya Kitaifa itayokuwa ikifanyika kila mwaka Mpoto amesema kuwa lengo kubwa ni kurejesha hali ya Uzalendo na Utaifa katika kutatua changamoto zilizojitokeza na zitakazojitokeza nchini.

“Usiku wa Kitendawili utatumika kama jukwaa la kuwaleta pamoja watanzania pamoja na viongozi wao ili kukumbushana kuhusu wajibu na kujadili mustakabali wa Taifa,”amesema Mpoto.

 

Aidha, amesema lengo kuu la maadhimisho hayo kuambatana na maadhimisho ya kifo cha Baba wa Taifa kuanzia mwaka 2018 ni kutumia jukwaa hilo kufikisha ujumbe wa umuhimu wa kujenga na kuendeleza Utaifa.

Hata hivyo, ameongeza kuwa baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo wiki hii huko Dodoma, itafanyika kwenye mikoa yote nchini.

Magazeti ya Tanzania leo Desemba 5, 2017
Video: Mtulia akabidhiwa kadi ya CCM, anena makubwa