Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Innocent Bashungwa amewataka Viongozi kuhakikisha wanafuatilia na kusimamia kikamilifu matumizi ya Mfumo wa Anwani za Makazi ili kusaidia upatikanaji wa huduma kirahisi kwa wananchi.
Bashungwa amesema hayo leo Jijini Dodoma mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwenye kikao kazi cha Wakuu wa Mikoa kuhusu mfumo wa anwani za makazi amesema, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeshirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutoa maelekezo kwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa utekelezaji wa anwani za makazi.
Amesema kwa majukumu yaliyotekelezwa na Wizara kwa kushirikiana na wadau kuhusu anunwani za makazi ni pamoja na kuandaa miongozo ya mfumo wa anwani za makazi, kutunga sheria ndogo, utambuzi wa majina ya mitaa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa 184 Nchi nzima, kuandaa ramani za mipaka ya kiutawala, kujumuisha masuala ya mfumo wa anwani za makazi kwenye mwongozo wa mpango na bajeti katika mfumo wa undaaji wa bajeti.
Aidha Waziri Bashungwa amemuhakikishia Rais Samia kuwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI itaendelea kuratibu na kusimamia anunwani za makazi zinatekelezwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na wadau ifikapo Mei,2022 kama ilivyoainishwa katika mpango husika na uandaaaji wa ramani msingi na kuanzia ngazi ya kitongoji, mtaa, kata mpaka Mkoa.
Hata hivyo amezielekeza Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha zinashirikiana na wadau kuandaa majina ya barabara na mitaa na kuziwasilisha Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
“Ninazielekeza Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhamasisha wananchi na wadau washiriki katika usimakaji wa nguzo za majina ya barabara na mitaa, kubandika vibao vyenye namba za nyumba na mitaa” amesema Mhe. Bashungwa.