Kocha wa timu ya taifa ya Uswisi, Vladimir Petkovic amesema kuwa kikosi chake kimejipanga kumbana mbavu mshambuliaji wa Brazil, Neymar da Silva pamoja na safu ya washambuliaji wengine wa timu hiyo.
Alisema kuwa moja kati ya mbinu ya kuwafunga Brazil ni kuwavuruga mapema ili wafanye makosa ambayo yatatengeneza nafasi ya kuwapiga.
“Tutakuwa tumejipanga kwa kiasi cha kutosha, unatakiwa kuichanganya timu kama Brazil ili ifanye makosa ambayo yatakupa nafasi ya kuzifikia nyavu zao; na hiyo ndiyo mbinu ya kisaikolojia tutakayoitumia kwa sababu tunapaswa kufunga goli moja au mawili ili tushinde,” alisema.
Kocha huyo alisisitiza kuwa wanaingia uwanjani leo kwa lengo la kushinda mechi na sio kushiriki kama wapweke.
Naye nahodha wa timu hiyo, Stephan Lichtsteiner alieleza jinsi watakavyojaribu kumzuia Neymar asiguse nyavu zao, jambo ambalo alikiri ni kibarua kigumu pia.
“Haiwezekani kumdhibiti mchezaji kama Neymar kwa dakika zote 90, ni mchezaji aliyekamilika zaidi kwenye kiwango cha dunia,” alisema Lichtsteiner.
“Tunatakiwa kutumia uimara wetu, kutumia safu ya ulinzi, tunatakiwa kuziba nafasi zote mbele kwa wachezaji wengine pia wakati ambapo tunajaribu kumdhibiti mchezaji mmoja mwenye kiwango kama hicho [cha Neymar],” alisema.
Brazil na Uswisi wanakutana leo kwenye mchezo wao wa ufunguzi wa kundi E nchini Urusi, wakati ambapo Brazil bado inarekodi ya kubamizwa goli 7-1 na Ujerumani mwaka 2014, bila Neymar.
Uswisi wataingia uwanjani leo wakiwa na rekodi nzuri, ikiwa imepoteza mchezo mmoja pekee kati ya mechi 22 za mwisho katika kipindi cha miaka miwili. Kipigo pekee ilichowahi kupokea katika katika kipindi hicho ni kutoka kwa mabingwa wa Ulaya, Ureno.
Brazil ambao ni mabingwa mara tano, pia inaingia uwanjani ikiwa na rekodi nzuri ya kushinda michezo 17 kati ya mechi 21 chini ya kocha Tite, wakiwa kati ya timu zilizopewa matumaini ya kushinda kombe hilo.