Wakati kukiwa bado na sintofahamu na mvutano kuhusu uamuzi wa Serikali kukatisha matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge kupitia vituo vya runinga na radio, utafiti wa Twaweza umeonesha hitaji kubwa la wananchi.

Utafiti huo uliofanywa Tanzania bara ukihusisha sampuli ya wananchi 1,815 kwa uwakilishi wa kitaifa umebaini kuwa asilimia 88 ya wananchi wanataka Bunge lirushwe moja kwa moja kupitia vituo vya runinga na radio.

Utafiti huo ulifanyika kuanzia tarehe 29 Machi hadi tarehe 12 Aprili mwaka huu kwa kukusanya takwimu kwa njia ya simu na kupewa jina la ‘Sauti za Wananchi’, ukiwa ni utafiti wa kwanza kufanyika barani Afrika kwa njia hiyo ukiwa na uwakilishi wa kitaifa.

Kwa mujibu utafiti huo, kati ya wananchi waliokuwa wakifuatilia vikao vya Bunge moja kwa moja kabla ya kusitishwa, asilimia 60 walikuwa wakifuatilia kwa njia ya radio na asilimia 40 walikuwa wakifuatilia kupitia vituo vya runinga.

Akizungumzia utafiti huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze amesema kuwa umeonesha dhahiri shauku kubwa ya wananchi kutaka kuwaona na kuwasikia wabunge wao wakiwa wanawawakilisha Bungeni.

“Je, serikali iko tayari kuyapokea matakwa ya watanzania walio wengi katika jambo hili? Alihoji Eyakuze.

“Ikibadilisha maamuzi yake na kurudisha matangazo haya itakua ishara nzuri ya nia yake ya kuimarisha uhusiano wa karibu zaidi kati ya wananchi na wabunge wao,” aliongeza Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Twaweza.

Mvua kubwa imenyesha na mafuriko kufanya uharibifu mkubwa China
Video: Mkuu wa Mkoa DSM, Makonda amepokea milioni 100 kutoka CRDB