Imebainika kuwa baadhi ya wafungwa, hasa wale wa makosa madogomadogo kwenye gereza la Serikali la Hindi, Kaunti ya Lamu – Kenya, wamekuwa wakifanya uhalifu kwa makusudi punde wanapoachiliwa huru, wakidhamira kushtakiwa tena ili warudishwa jela, waendelee kufaidi huduma za bure za serikali wakiwa kifungoni.
Akizungumza kwenye gereza la Hindi, Afisa Msimamizi wa Magereza Kaunti ya Lamu, Festo Odongo alisema miongoni mwa huduma zinazowasukuma mahabusu wa zamani kutekeleza uhalifu na kurudi jela ni matibabu, chakula, ulinzi, malazi na ‘starehe’ nyingine ambazo wafungwa hao wanazipata gerezani.
Odongo amesema, kuna maradhi ambayo baadhi ya wafungwa huugua na ni ghali kuyatibu na hivyo kuhitaji uangalizi wa karibu kimatibabu kitu ambacho hupelekea wengi wao kufanya visa kwa makusudi ili warejee tena Gerezani.
Amesema, kwa mujibu wa utaratibu wa nchi ni haki kwa wafungwa wanapokuwa gerezani wapate tiba wanapougua, na wamedhirihirisha hilo baada ya kufanya uchunguzi wa kina na pia kwa kuthibitisha toka miongoni mwao ambao wamekuwa wakirejea mara baada ya kuachiliwa.