Utafiti uliofanywa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Tanzania Development Initiatives (Tadip), umeonesha kuwa kama kura zingepigwa kati ya Septemba 1 na Septemba 23, mgombea urais kupitia Chadema, Edward Lowassa angeshinda kwa asilimia 54.4.

Kwa mujibu wa utafiti huo uliohusisha watu 2500 waliojiandisha katika daftari la kupiga kura kwa njia ya BVR katika mikoa 12 nchini, Lowassa anafuatiwa na mgombea urais kupitia CCM, Dk John Magufuli aliyepata asilimia 40 huku mgombea wa ACT – Wazalendo, Anna Mgwira akipata asilimia 2.

Mgombea wa Chaumma, Hashim Rungwe amepata asilimia 0.4, mgombea wa ADC, Chief Yemba amepata asilimia 0.1 huku asilimia 3 ya wananchi wakisema bado hawafahamu nani watakayempigia kura.

Mkurugenzi wa Tadip, George Shumbuso aliwaambia waandishi wa habari kuwa utafiti huo ulifanywa kwa kutumia madodoso yaliyogawiwa kwa wasitani wa mtu 1 kwa kila baada ya nyumba 20, ambapo kati ya madodoso 2500 yaliyogawiwa, madodoso 2040 yalijazwa na kurejeshwa.

Alisema waliamua kuchagua mikoa hiyo 12 kulingana na takwimu za NEC zinazoonesha kuwa mikoa hiyo ndiyo yenye wapiga kura wengi zaidi.

Utafiti huo unaonesha kuwa Edward Lowassa anapendwa zaidi na vijana pamoja na wanaume huku Dk John Magufuli akipendwa zaidi na wanawake na wazee. Mgombea wa ACT-Maendeleo pia amebainika kuungwa mkono kwa wingi na wanawake.

Katika mikoa hiyo iliyofanyiwa utafiti, Lowassa ameonekana kuongoza zaidi katika mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha na Tanga huku Magufuli aking’ara zaidi kwenye mikoa ya Dodoma na Morogoro.

Utafiti uliotolewa awali na Taasisi ya Twaweza ulimpa Magufuli ushindi wa asilimia 65 dhidi ya Lowassa aliyepata 25 huku IPSOS wakimpa Magufuli ushindi wa asilimia 62 dhidi ya Lowassa alipewa asilimia 31.

Matokeo ya utafiti wa Twaweza yalikosolewa vikali na wasomi na wananchi mbalimbali hasa baada ya kuonekana baadhi ya maeneo jumla y asilimia zikifika 101 hadala ya asilimia 100. Pia, njia ya kukusanya taarifa kwa kutumia simu na kuwapa simu pamoja na chaja watoa taarifa ilionekana kuwa sehemu ya changamoto.

 

Lowassa Awaelekeza Wananchi Jinsi Ya Kuwajibu 'Wanaomtukana'
Tanzania Mwenyeji Wa Kozi Ya Waamuzi Afrika