Wakati matokeo ya tafiti mbalimbali yanaendelea kutolewa kuhusu uchaguzi mkuu wa Kenya, matokeo ya utafiti mpya uliofanywa na ‘Infotrak’ unaonesha mgombea wa kambi ya upinzani ya NASA, Raila Odinga angepata ushindi mwembamba dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta kama uchaguzi ungefanyika jana.
Matokeo hayo ya utafiti yanaonesha kuwa Raila alipata asilima 49 dhidi ya Kenyatta ambaye alipata asilimia 48. Mgombea wa Tunza, Abduba Dida angepata asilimia 0.3 na Ekuru Aukot angepata asilimia 0.1 ya kura zote; na asilimia 2 walisema bado hawajafanya maamuzi.
Akisoma matokeo ya tafiti hizo jijini Nairobi, Afisa Mtendaji Mkuu wa Infotrak, Angela Ambitho alisema kuwa utafiti huo ulifanyika kwa kuchukua sampuli kutoka kwenye daftari la wapiga kura la Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC).
“Tulifanya mahojiano na watu ambao wamesajiliwa kwenye daftari la wapiga kura ambao waliweka wazi kuwa watapiga kura,” alisema Ambitho.
- Mkojo wa Masogange watetewa kama wa Wema, yadaiwa una ‘Unga’
- UN yatoa ripoti ya hali ya kisiasa nchini Burundi
Utafiti huo uliowahusisha wapiga kura 5,000 ulionesha kuwa Raila anaongoza zaidi katika maeneo ya Pwani, Mashariki, Magharibi, Nyanza na Nairobi wakati Kenyatta akiongoza maeneo ya Rift Valley, Kusini Mashariki na Mikoa ya Kati.
Kenya inatarajia kufanya uchaguzi mkuu Agosti 8 mwaka huu, uchaguzi unaotajwa kuwa wa ushindani mkubwa kuwahi kutokea katika historia ya nchi hiyo.