Tatizo la upweke ambalo linawakumba watu wengi hasa wenye umri wa zaidi ya miaka 50, litawaumiza mamilioni zaidi duniani ndani ya kipindi cha muongo mmoja, kwa mujibu wa utafiti wa hivi karibuni.
Utafiti huo uliofanywa na Shirika la Age UK, likitumia nchi hiyo kama sampuli, umeonesha kuwa kutokana na kuongezeka kwa kwa kasi kwa idadi ya wazee ukilinganisha na wastani wa ongezeko la makundi mengine, watu wanaoishi wakisongwa na tatizo la upweke wataongezeka kwa zaidi ya nusu milioni kwa Uingereza pekee.
Shirika hilo limetahadharisha kuwa upweke ni tatizo ambalo linaweza kuwa na madhara makubwa kwa afya ya binadamu.
“Idadi ya watu wenye umri mkubwa inaongezeka kwa kasi hivyo tunaelekea kuwa na watu zaidi ya milioni mbili wenye tatizo sugu la upweke katika kipindi kisichozidi miaka kumi. Pia, wakiwa na madhara makubwa ya kiakili na kimwili, hivyo tunapaswa kuchukua hatua,” Mkurugenzi wa Age UK, Caroline Abrahams alisema.
Kwa mujibu wa ripoti, watu wenye umri wa zaidi ya miaka 50 wana uwezekano mkubwa wa kukumbwa na upweke kama; hawatakuwa na watu wa kuzungumza nao wanapohitaji kufanya hivyo, wakiwa wajane au kuachika, wakiwa wanahisi hawana uhusiano na majirani na kutokuwa na uwezo wa kufanya kile walichokuwa wanafanya ili kuishi peke yao.
Utafiti huo umeeleza kuwa wajane na wagane wana uwezekano mara tano wa kupata upweke zaidi ukilinganisha na watu wenye umri huo waliopo kwenye uhusiano wa mapenzi.
Huenda Tanzania pia inapaswa kulikumbuka neno la Rais John Magufuli kuwa endapo watu watashauriwa sana kuhusu kuacha kuzaa watoto wengi, kuna hatari mbeleni idadi ya wazee ikawa kubwa kuliko vijana na watoto.