Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania (TALIRI), Dkt. Jonas Kizima amesema wanafanya utafiti ambao umejikita katika kutatua changamoto za mbegu bora za mifugo na mbegu bora za malisho kwa wafugaji ili sekta ya mifugo iweze kuchangia vyema katika pato la Taifa.
Dkt. Kizima ameyasema hayo alipotembelea kukagua shughuli zinazofanywa na Kituo cha TALIRI Mpwapwa kilichopo Wilayani Mpwapwa, Mkoani Dodoma Februari 18, 2021.
Amesema kuwa lengo la utafiti wanaoufanya ni kuhakikisha wanapata mbegu bora za mifugo na kuzalisha mbego bora za malisho ya mifugo ambazo zitasaidia kutatua changamoto za upatikanaji wa mbegu bora za mifugo zinazohimili mazingira yaliyopo na malisho inayoikabili nchi kwa sasa.
Ameongeza kuwa kwa sasa taasisi hiyo inaendelea na kufanya tathmini ya ubora, ustahimilivu na makuzi ya malisho ya mifugo yatakayofaa kwa chakula cha kutosha kwa ajili ya mifugo.
“Tafiti tunazozifanya zinalenga kuimarisha mnyororo wa thamani wa mifugo ili mchango wa sekta ya mifugo uweze kuonekana katika uchumi wa kati,” amesema Dkt. Kizima.
TALIRI imesambaza vituo vyake katika Kanda Saba nchini ambazo ni Kanda ya Mashariki, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kati, Kanda ya Kusini, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Ziwa na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, ili kuwa karibu na wafugaji na kuwasaidia kutatua changamoto zao ili waweze kufanya ufugaji wenye tija.