Serikali wilayani Njombe imewataka watanzania kwenda katika wilaya hiyo kufanya utalii wa kuona hali ya baridi kali ambayo inaendelea kwa kipindi hiki.
Mkuu wa Wilaya ya Njombe amesema hali ya hewa ya eneo hilo kwa sasa ni ya kuvutia na amewataka wananchi kwenda kufanya utalii na kufurahia mazingira tofauti.
“Niwaombe Watu wengine nchini wanaotamani kuvaa nguo za baridi na wana swaga zao wameziweka ndani wazibebe waje njombe watafuarahia sana, Njombe ni eneo zuri sana la kufanya utalii wa baridi,”
Hata hivyo, serikali imeendelea kutoa wito kwa Wakazi wa Mkoa huo kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya baridi hiyo kwa kuvaa nguo nzito ili kujikinga na magonjwa yanayotokana na baridi.
Wakulima wametakiwa kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa katika Mamlaka husika ili ziweze kuwasaidia katika kilimo.
Hata hivyo hali hewa ya baridi kali katika baadhi ya maeneo mkoani humo imesababisha shughuli za kiuchumi kusimama kutokana na wakazi wa maeneo hayo wakiwemo wasafirishaji wa abiria kwa njia ya pikipiki (Bodaboda) kupunguza muda wa kufanya kazi huku wakitafuta vyanzo vya joto ikiwemo jiko la mkaa na kuota moto ili kupunguza baridi katika miili yao.
Afisa Mfawidhi katika kituo cha hali ya hewa kilichopo Igeli kata ya Luponde mkoani Njombe, Joseph Fumbo, amesema kwa kipindi hiki Mkoa wa Njombe huwa na baridi kali.
Pamoja na hayo amewataka wakazi wa eneo hilo kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kufuata utaratibu wa kujikinga na baridi huku wakiepuka kulala na moto wa jiko la mkaa ndani kwa kuwa umekuwa ukisababisha vifo.