Ubunifu wa kutumia puto kuzunguka eneo la Hifadhi ya Taifa ya Ruaha umekuwa kivutio kikubwa kwa watalii na kupendezesha shughuli ya utalii kwa ujumla katika eneo hilo.
Hifadhi ya Taifa ya Ruaha iliyoko mkoani Iringa imeanzisha utalii huo wa kutumia puto kwa wageni na watalii wanaofika ili waweze kuzunguka eneo kubwa la hifadhi hiyo na kuona mazingira ya hifadhi hiyo ambayo ni kubwa kuliko zote Afrika.
Ofisa utalii na masoko katika hifadhi hiyo, Antipas Mgungusi amebainisha hayo kwa waandishi wa habari za Mazingira (JET), waliofika katika hifadhi hiyo kwa ajili ya kupata uelewa katika masuala mbalimbali ya uhifadhi.
Mgungusi amesema utalii wa kuruka kwa kutumia puto katika hifadhi hiyo ulianzishwa mwaka jana na unaendeshwa na kampuni binafsi hatua inayolenga kuwafikisha watalii maeneo ya mbali zaidi na kuona vivutio vya hifadhi hiyo kwa urahisi.
“Marubani wa puto hizo wanayafahamu vizuri mazingira ya hifadhi, hivyo huwafikisha watalii maeneo yote yanayovutia,” alisema Mgungusi na kuongeza, “na kwa kutumia aina hii ya utalii, Ruaha tunatarajia kuongeza idadi ya watalii wanaoruka angani.”
Ameongeza kuwa katika puto moja wanaingia wageni 12 ambao wanaweza kuzunguka kwa wastani wa saa moja, na kwamba wana mpango wa kuanza kutumia mfumo wa boti kutembeza watalii ifikapo 2020.
Hifadhi ya Ruaha ipo kilomita 130 kutoka mjini Iringa na ina viwanja vidogo vya ndege vinavyopokea watalii. Na ni ya pili katika kutumia puto katika utalii baada ba Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.