Duniani kuna Makabila mengi ambayo yana utamaduni wake, lakini baadhi ya tamaduni za makabila hayo zimekuwa zikishangaza na kuacha maswali, kutokana na utaratibu husika wa maisha yalivyo.
- Kuibiana wake
Huko Niger, Taifa linalopatikana Magharibi mwa bara la Afrika kuna Kabila la Wodaabe ambalo lina utaratibu wa maisha unaoshangaza kwani Wanaume hujulikana kwa kuibiana wake. Ipo hivi, ndoa ya kwanza ya Wodaabe hupangwa na wazazi wao wakati watoto wao wakiwa wachanga na lazima iwe baina ya watu wa ndani ya ukoo huo.
Watoto hao wanapokuwa na kubalehe huwa na fikra au hisia tofauti kalini hulazimika kuoana hata kama hawapendani ili kutimiza mila, sasa kuliepuka hili huwa linaandaliwa Tamasha la kila mwaka likifahamika kwa jina la Gerewol, hapo Wanaume wa Wodaabe hujipodoa na kuvalia mavazi nadhifu ya kimila na kucheza kwa umahiri Dansi ili kuwavutia Wanawake.
Wakati usakataji wa Dansi ukiendelea, Mwanamume hufanya mbinu ili aweze kumuiba msichana ampendaye hata kama ameolewa lakini bila kutambuliwa (hasa kwa zile ndoa ambazo Mume hataki kuachana na mkewe), basi ikiwa atafanikiwa kumtorosha bila kufahamika, huo unakuwa ni ushindi kwake na watatambulika rasmi kwa jamii bila kelele, ugomvi ama kushitakiana.
Bado tunaangazia tamaduni za Makabila na taratibu zao ambazo zimekuwa zikishangaza na kuacha maswali, kutokana na utaratibu husika wa maisha yao jinsi yalivyo.
- Ukitema mate umemsalimia mwenzio
Kabila la Wamasai linalopatikana Kenya na Tanzania (kwa baadhi ya Wamasai), wana utamaduni wa kutema mate kama njia ya kusema hello. Kwa Wazungu wangelikutana basi wangelipeana salamu kwa kutamka neno Hello!!.. lakini kwa Mmasai kutema mate ni njia mojawapo ya kusalimiana.
Tukio kama hili, pia hufanyika mtoto mchanga anapozaliwa, yaani ni desturi kwa Wanaume kumtemea mate mtoto mchanga na kumnenea kuwa ni mbaya kitu ambacho hushangaza, wao wanaamini kuwa njia hii ingemlinda mtoto kutokana na hila za walimwengu na roho zilizo ovu.
Mashujaa wa Kimasai pia hutemea mate mikononi mwao kabla ya kupeana mkono wa mzee. pia ni jadi yao au utamaduni wao kunywa damu safi ya wanyama, wakiamini kufanya hivyo ni ushujaa ingawa matendo haya si kwa wamasai wote bali baadhi ya koo na si kwa rika zinazoshabihiana, isipokuwa kuna umri wake.
Pia Wamasai wana saalaam zao ambazo mtu mwingine yeyote hawezi gundua huku wakitumia fimbo kupeana ishara za mambo mbalimbali ikiwemo njaa mtu anapohitaji chakula, kutambuana au kugundua endapo ni kweli mtu anayewasiliana naye ni Mmasai au alimdanganya, ambapo kitakachomfanya apate utambuzi ni matokeo baada ya kumfanyia ishara.
Itaendelea.