Jana, ilizuka taharuki baada ya kuripotiwa kukamatwa kwa vifaa vilivyosadikika kuwa ni vile vilivyotumika kuandikisha wapiga kura kwa njia ya kieletroniki (BVR) vilivyokutwa katika kiwanda cha MM Steel cha Dar es Salaam.

Uongozi wa kiwanda hicho ulikuwa unaendelea na zoezi la kuandikisha wafanyakazi hao kwa njia ya kielekroniki kwa kuchukua alama zao za vidole kama ilivyokuwa kwenye zoezi la BVR, hali iliyowashtua wafanyakazi hao.

Taarifa hizo zilieleza kuwa baada ya kupata taarifa, Jeshi la Polisi, NEC, pamoja na viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mwanasheria wa chama hicho, John Mallya walifika kiwandani hapo.

Kwa mujibu wa Meneja Mawasiliano wa Kampuni hiyo, Abubakari Mlawa, viongozi wa Chadema ndio waliokuwa wa kwanza kufika katika eneo hilo na kuwaweka chini ya ulinzi kisha jeshi la polisi pamoja na viongozi wa NEC waliwasili baada ya kupata taarifa.

Walipohojiwa kuhusu vifaa hivyo, Meneja Mawasiliano wa Kampuni hiyo alieleza kuwa vifaa hivyo havina uhusiano na zoezi la upigaji kura na kwamba wanachukua alama za vidole vya wafanyakazi hao kwa nia ya kuimarisha ulinzi kiwandani hapo na sio vinginevyo.

“Tunaendelea na zoezi la kuweka data base kwa ajili ya wafanyakazi wetu wote kwa maana ya kupiga picha na kuandika taarifa zake zote. Amezaliwa wapi, amesoma wapi, ameanza kazi lini,” alisema Mlawa.

“Tunafanya zoezi hili wiki nzima na tumeandikisha wafanyakazi zaidi ya 100 na tuna zaidi ya wafanyakazi 900,” aliongeza.

Kwa upande wake, afisa wa ICT wa NEC, Amosi Mahda alisema kuwa ni mapema sana kueleza kama vifaa hivyo ni vya BVR au la hadi pale vitakapochunguzwa zaidi.

NEC, Chadema na Polisi walikubaliana kuwa vifaa hivyo vipelekwe polisi kwa ajili ya uchunguzi ili kubaini ukweli.

“Tutatoa taarifa mapema na kwa wakati ili kuondoa wingu lililotanda kwa sasa, tunataka pande zote zijiridhishe hivyo tutafanya kwa uwazi kueleza kama hizi ni mashine zetu au la,” alisema Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango ya NEC.

Hata hivyo, Meneja Mawasiliano wa kampuni ya MM Steel, alishindwa kufafanua kuhusu njia zilizotumika kununua mashine hiyo. Alieleza kuwa mashine hiyo ilinunuliwa kutoka nje ya nchi kupitia tenda waliyolipa kampuni fulani. Hata hivyo, alishindwa kutaja kampuni waliyoipa tenda hiyo.

Dar24 iliongea na mmoja kati ya wafanyakazi wa MM Steel, ambaye alieleza kuwa wafanyakazi wa kiwanda hicho walitaka kuligomea zoezi hilo lakini walilazimishwa na kuelezwa kuwa ambao wanataka kuendelea na kazi sharti wapange foleni wajisajili kwenye mashine hizo.

“Zoezi la kusajili pamoja na mashine inayotumika vinafanana kabisa na uandikishaji wa BVR, ni vilevile. Ndio maana tukashtukia mpango,” alisema mfanyakazi mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.

 

 

 

 

Chelsea, Arsenal Zaadhibiwa Na FA
Messi Kusimamishwa Kizimbani