Amber Rutty ambaye anakabiliwa na kitanzi cha Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015 pamoja na tuhuma za kufanya kosa la mapenzi kinyume cha maumbile kufuatia video yake chafu iliyoonekana mtandaoni ameeleza anachoamini kuwa ni utetezi wake.
Msichana huyo ambaye alijisalimisha katika kituo cha polisi baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda pamoja na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola kumtaka afanye hivyo ndani ya saa 12, amedai kuwa video hizo zilivujishwa mtandaoni na mwizi wa simu.
Akihojiwa dakika chache kabla hajaingia katika kituo cha polisi cha Wilaya ya Kipolisi ya Mbagala, msichana huyo alidai kuwa alirekodi video hizo akiwa faragha na mpenzi wake, kwa kutumia simu ya mpenzi wake ambayo iliibiwa siku chache baadaye.
“Baada ya wiki ya tatu, mpenzi wangu aliibiwa simu na hizo video zilikuwa kwenye memory card. Kwahiyo baada ya muda ndio huyo mtu amechukua hivyo vitu akavisambaza,” alisema.
Alidai kuwa wakati wanarekodi video hizo alikuwa amelewa pamoja na mpenzi wake huyo ambaye aliambatana naye katika kituo hicho cha polisi.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015, Kifungu cha 14 kinachozungumzia ponografia, ni kosa kuchapisha au kusababisha kuchapishwa kwa picha/video za ponografia ya kiasherati au chafu.
Sheria hiyo inaeleza wazi kuwa mtu atakayekutwa na hatia ya kusababisha au kusambaza picha za ponografia ya kiasherati au chafu atalipa faini ya shilingi milioni thelathini au kifungo kisichopungua miaka kumi au vyote kwa pamoja.
Hivyo, kwa mujibu wa tafsiri za wanasheria, kurekodi picha zilizo kinyume na maadili, picha za faragha na za ponografia ni kosa.
Katika hatua nyingine, mwanasheria Alberto Msando amesaidia kutoa ufafanuzi wa tuhuma zinazomkabili Amber Rutty, endapo atakutwa na hatia ya kufanya mapenzi kinyume cha maumbile atakumbwa na adhabu ya kifungo cha maisha au miaka 30 jela.
Oktoba 26, Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) lilieleza kutomtambua Amber Rutty kama msanii hivyo likaviachia vyombo vya dola.