Beki wa klabu ya AFC Bournemouth, Tyrone Mings amefungiwa kucheza michezo mitano inayoratibiwa na Chama chaSoka nchini England/Uingereza (FA), baada ya kukutwa na hatia ya kumkanyaga kwa makusudi mshambuliaji wa Man Utd, Zlatan Ibrahimovic.
Mings alifanya tukio hilo wakati wa mchezo wa ligi kuu uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita kwenye uwanja wa Old Trafford. Hata hivyo, alipowasilisha utetezi wake mbele ya FA alizikana tuhuma hizo.
Katika utetezi wake, beki huyo mwenye umri wa miaka 23, alidai hakumkanyaga kwa makusudi mshambuliaji huyo kutoka nchini Sweden bali alikuwa katika harakati za kuukwepa mkono wa Zlatan lakini kwa bahati mbaya alimkanyaga kichwani.
Maamuzi hayo ya FA yameusikitisha uongozi wa AFC Bournemouth ambao umedai ni pigo kubwa sana kwao kumkosa Mings katika michezo mitano, ambayo itakuwa na umuhimu mkubwa.
Mings ataanza kuitumikia adhabu yake mwishoni mwa juma hili kwa kukosa mchezo dhidi ya West Ham, kisha Swansea (Machi 18), Southampton (Aprili Mosi), Liverpool (Aprili 5) na Chelsea (Aprili 8).
Mings anaratajiwa kurejea uwanjani Aprili 15 ambapo AFC Bournemouth itakuwa na kibarua cha kuwakabili Tottenham.
Hata hivyo, rungu la FA halikumshuia Mings peke yake bali limemtwanga pia Zlatan Ibrahimovic ambaye alikuwa amefunguliwa mashataka ya kumpiga kiwiko Mings, kitendo ambacho kilitazamwa kama kurudisha mashambulizi. Mchezaji huyo wa Mashetani Wekundu amefungiwa michezo mitatu.