Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU, Gerson Msigwa ilieleza kuwa Rais Magufuli baada ya kutengua uteuzi wa Mramba, amemteua Dk Tito Mwinuka kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco.

Mwinuka ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) na hadi uteuzi wa jana, alikuwa ni Mkuu wa Idara ya Mekanika na Uhandisi wa Viwanda Chuo cha Uhandisi na Teknolojia (CoET) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Akiwa kanisani, Rais Magufuli alimpongeza Profesa Muhongo kwa hatua ya kusimamisha kupanda kwa bei ya umeme. “Namshukuru waziri wa nishati kwamba ameshatengua maamuzi hayo, kwa hiyo umeme hakuna kupanda.”

Rais Magufuli alisema haiwezekani watu mnapanga mikakati ya kujenga viwanda na hasa katika mikakati hii mikubwa ya nchi ya kusambaza umeme hadi vijijini na umeme huo unaenda hadi kwa watu maskini walioumbwa kwa mfano wa Mungu, halafu mtu pekee kwa sababu ya cheo chake anakwenda kusimama kupandisha bei ya umeme.

Akionekana kukereka kwa hatua hiyo ya kupandishwa kwa bei ya umeme, Rais Magufuli alisema, “Na ndio maana baba askofu nalizungumza hili kwamba majipu bado yapo na nitaendelea kuyatumbua, ndio maana naomba sana Watanzania muendelee kutuombea, lengo la serikali ninayoiongoza ni kwenda na wananchi wa kipato cha chini.”

Chadema: Tumejipanga kuchagua viongozi makini
Kisa cha Mramba kufukuzwa kazi