Scolastica Msewa – Pwani.
Mitungi ya majiko ya gasi ya Kampuni ya Oryx 3600 imegaiwa kwa Wananchi wa Mkoa wa Pwani, ikiwa ni mpango wa Kampuni hiyo kuunga mkono jitihada za Serikali za kuthibiti ukataji miti na utunzaji wa mazingira na kupunguza matumizi ya kuni na mkaa.
Akitoa mada kwa Wafanyabishara wauza gasi za Oryx wa Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani Afisa Masoko wa Oryx, Evarest Kisaka amesema mitungi hiyo imetolewa kwa ushirikiano na Wakala wa Umeme vijijini – REA, ambao walitoa mitungi 1800 na Kampuni hiyo kutoa mitungi 1800.
Amesema, mitungi hiyo imekabidhiwa kwa Wabunge wa majimbo ya mkoa wa Pwani ambao wataigawa kwa Wananchi wakilenga kudhibiti ukataji miti na utunzaji wa mazingira ambao utasaidia kupambana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo hupelekea uhaba wa mvua na kuleta athari kwa jamii.
“Tunajua wote kwamba mvua zisiponyesha njaa inakuwa kali na njaa ikishakuwa kali ni mzigo kwa taifa hivyo Serikali inapambana kutoa elimu na kutoa mitungi ya majiko ya kuanzia kwa Wananchi wasio tumia gasi lengo tu Watanzania tuachane na matumizi ya nishati isiyo rafiki,” amesema Kisaka.
Naye Afisa Masoko wa Kampuni ya ECO Africa, Abdullatif Jafar Abeid amewataadhalisha Watumishi wa majiko ya gasi kuzingatia vifaa vyenye ubora, itakayosaidia kujilinda na matukio ya moto majumbani kwa kuiweka mita zaidi ya mbili kutoka kwenye jiko, ili kujihakikisha usalama wao na Mali.
Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Mkuranga, Francisco Chunji aliwataka Wafanyabiashara ya uuzaji wa mitungi ya gasi kufika kwenye Ofisi zao ili kupata elimu ya namna sahihi ya kutoa huduma kwa Wananchi.