Kiongozi wa ngazi ya juu nchini Uturuki, Yasin Aktay, amesema kuwa anaamini kuwa mwili wa mwandishi, Jamal Khashoggi uliyeyushwa kwenye tindikali baada ya kuuawa na kukatwa katwa.
Atkay ambaye ni mshauri wa Rais wa Uturuki, Recep Erdogan Tayyip amesema hitimisho pekee linaloingia akilini ni kuwa waliomuua mwandishi huyo wameteketeza mwili wake ili kufuta ushahidi.
Khashoggi, ambaye alikuwa mkosoaji mkuu wa utawala wa Saudia Arabia hususani sera za mrithi wa kiti cha ufalme mwanamfalme, Mohammed bin Salman aliuawa ndani ya ubalozi mdogo wa Saudia jijini Istanbul Oktoba 2 mwaka huu.
“Sababu ya kumkata vipande vipande ilikuwa ni kurahisisha kuyeyusha mwili huo kwa wepesi, na sasa tumefahamu kwamba mwili wake uliyeyushwa ili kupoteza ushahidi,”amesema Aktay alipokuwa akifanya mahojiano na gazeti la kila siku la Hurriyet.
Hata hivyo, Khashoggi alikimbilia Marekani mwaka 2017 akihofia usalama wake na huko alikuwa akiandika makala na maoni kwenye gazeti la Washington Post.