Shirika la ndege la kitaifa la Kazakhstan Air Astana na shirika la ndege la Uturuki la Pegasus leo hii yamesimamisha kwa muda safari za ndege kwenda Urusi, kufuatia vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Moscow kutokana na kile inachokiita “operesheni ya kijeshi” nchini Ukraine.
Katika taarifa zao zilizotolewa kwa vyombo vya habari, hatua hiyo inatokana na kutokuwa na uhakika juu ya bima ya usalama wa safari za ndege zinazoelekea Urusi.Wakati shirika Astana likisema litarejesha safari hizo hivi karibuni, lile la Uturuki limesema limesimamisha kuanzia Machi 13 hadi 27.
Hali hiyo inatokana na vikwazo vya mataifa ya Magharibi, kutokana na kutotumika tena kwa bima za operesheni za makampuni ya ndege.Uingereza, Canada na Umoja wa Ulaya na Marekani zimesitisha pia safari zake za ndege na kuifunga kabisa anga kwa ndege za Urusi ikiwa kama sehemu ya vikwazo. Urusi nayo imechukua hatua kama hiyo kwa anga yake kwa kulipiza kisasi.