Mazungumzo yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa yenye lengo la kuteua serikali ya mpito nchini Libya ili kukomesha mzozo ambao umedumu kwa muongo mzima sasa, yamemalizika bila ya kuutaja uongozi wa serikali hiyo.
Kaimu Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa Libya, Stephanie Williams, amewaambia waandishi wa habari kwamba wameamua kuendelea na mkutano mwingine ndani ya wiki moja, kuhusu jinsi ya kuupata uongozi huo.
Mkutano huo wa wiki moja, ambao ndio hatua ya hivi karibuni zaidi katika kutafuta suluhisho la kisiasa kwa mzozo wa Libya, uliwahusisha wajumbe 75 waliochaguliwa na Umoja wa Mataifa kuwakilisha makundi muhimu ya Libya.
Wajumbe hao walipewa jukumu la kubuni mpango wa kuipeleka Libya kwenye uchaguzi, kuamua juu ya mamlaka utakayokuwa nayo uongozi wa serikali ya mpito na kuwataja wajumbe wa serikali hiyo.
Mazungumzo ya sasa yanafanyika wakati Libya ikiwa kwenye shinikizo kubwa la kimataifa kuumalia mzozo ambao unakaribia miaka kumi sasa, tangu kupinduliwa na kuuawa kiongozi wa taifa hilo la kaskazini mwa Afrika, Muammar Gaddafi.