Umoja wa vijana wa Chama cha Mapinduzi CCM, (UVCCM), umesema bila ya misingi ya Chama cha Mapinduzi ya utawala bora, haki na Demokrasia chini ya Serikali ya CCM, kutoundwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar au kutokea Mapinduzi ya Zanzibar,hali ya usalama na amani nchini ingekuwa tete na umoja wa kitaifa ungevurugika.
Umoja huo umesisitiza kuwa CCM na Serikali zake ndio zilizoijenga misingi hiyo, sera za uhakika,mahusiano ya kijamii ikipinga siasa za ubaguzi,kukomesha ukabila, ubaguzi,unyonyaji na umwinyi vinginevyo Tanzania ingekuwa kama Somalia.
Hayo yamesemwa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Mharamba kata ya Nkome, Wilaya ya Geita, mkoani Geita, amesema kuwa fikra, mtazamo na matumaini ya wakoloni na vibaraka walisubiri kuviona vyama vya TANU na ASP vikishindwa kuongoza dola ili wapate ya kusema.
“Wanaopiga kelele sasa wanapaswa kusoma historia bila CCM, iliyotokana na TANU,ASP uwepo wa sera makini na misimamo thabiti ya kitaifa na kimataifa, nchi ingetetereka kama yalivyotikisika mataifa mengine barani Afrika,lazima tukubali kuishi kwa kufuata sheria na kuheshimu mamlaka ya dola.”amesema Shaka.
Kwa upande wake Mgombea wa kiti cha udiwani wa Kata ya Nkome Masumbuko Malebesi, amesema kuwa kama akichaguliwa katika nafasi hiyo ya udiwani atawasilisha kero, matatizo na changamoto mahali husika ili ziweze kufanyiwa kazi na kupatiwa ufumbuzi.