Jumuiya ya Umoja  wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Njombe wameandaa mkutano maalum utakaoshirikisha vijana mbalimbali mkoani humo kujadili janga la mauaji ya watoto ambalo limeukumba mkoa huo.

Hayo yamesemwa mkoani humo na Katibu wa hamasa  na Chipukizi wa UVCCM, Jonson Mgimba alipokuwa akizungumza na Dar24 Media, ambapo amesema kuwa mkutano huo utalenga kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo.

”Sisi vijana wa UVCCM ndio walinzi wakubwa wa watoto hawa ambao wanauawa na hawa watu ambao sisi tunaamini tunaishi nao kwenye jamii zetu hali hii imetufanya tuendelee kujipanga zaidi,”amesema Mgimba

Aidha, amesema kuwa uongozi umewaalika vijana mbalimbali kushiriki katika mkutano huo ili kutoa maoni yao pamoja na kujipanga kukabiliana na wahalifu pindi wanaposafirisha abiria wanaokuwa na mashaka nao.

Pia ameongeza kuwa jamii inajukumu kubwa la kushiriki na kujiimarisha katika suala zima la ulinzi shirikishi kwa kusaidiana na vyombo vya ulinzi na usalama katika mkoa wa Njombe.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi mkoani humo wamepongeza juhudi za vijana hao na kusema kuwa jambo hilo ni jema kwakuwa vijana hao wakiamua kujituma kutetea wadogo zao wanaweza kuisaidia serikali katika kukabiliana na uhalifu huo.

 

Mawakili Njombe waomba kusogezewa Mahakama Kuu
CCM Njombe yaadhimisha miaka 42 ya chama kwa kupanda miche ya Chai