Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Ally Mohamed Kawaida ameiomba Wizara ya Kilimo kuongeza idadi ya vyuo vya Kilimo na kuvipandisha hadhi vilivyoachwa na waasisi wa Taifa kutoa elimu ya cheti hadi ngazi ya shahada ili kuchangie katika uzalishaji wa wataalamu wa kilimo na kukuza pato la taifa.
Kawaida ameyasema hayo katika ziara yake ya ukaguzi wa mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora – BBT, akiwa katika chuo cha mafunzo ya kilimo Mult Maruku, kilichopo Halmashauri ya Bukoba mkoani Kagera ambapo pia amewataka vijana kuchangamkia fursa zilizopo kwenye kilimo.
Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Ally Kawaida akiongozana na Mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Kagera Bruan Faris kwenda kukagua shamba la vijana wanufaika kupitia mradi wa BBT.
Amesema, “tuiombe wizara ya kilimo iangalie utaratibu wake kama itawezekana kupandisha hadhi vyuo vya kilimo kikiwemo chuo cha kilimo cha Mbeya -SUA, tunapozungumza kuasisi mazuri ya viongozi waliopita ni pamoja na kuviendeleza vile walivyoviacha ikiwezekana tuangalie na chuo kilichopo Mwanza ili kwa vijana wenzetu walio kanda ya ziwa nao wasisafiri masafa ya mbali kutafuta shahada ya kilimo.”
Awali, akisoma taarifa ya maendeleo ya mafunzo ya kilimo chuoni hapo, Mkuu wa chuo hicho Laurent Methew ameishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya awamu ya sita ya Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha mradi huo huku akisisitiza kuwa elimu hiyo inaenda kuleta mabadiliko kwa vijana hao.
Mwenyekiti wa Vijana Taifa (UVCCM) Ally Mohammed Kawaida akikagua moja ya shamba lililoandaliwa na vijana wa BBT.
Amesema, “hitaji kubwa ni kutoa elimu ya kilimo kwa vijana ili waweze kuwa na ajira ya kudumu, chuoni hapa serikali ya awamu ya sita tunashukuru kwa kuwezesha vijana 39 kupata elimu ya kilimo kupitia huu mradi wa BBT”.
Kwa upande wao vijana 39 wanaopata mafunzo hayo kwenye chuo cha Mafunzo Maruku wameeleza kuwa mafunzo hayo yamewabadilisha fikra zao kwa kuona kilimo ni biashara wala sio adhabu kwani wameshaona fursa zinazopatikana kupitia kilimo.