Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), umewavaa viongozi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kile walichodai kuendesha siasa za maigizo baada ya kushindwa kuzindua Operesheni UKUTA, Septemba 1.

Kupitia taaria yake kwa vyombo vya habari, Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, amesema kuwa Chadema walijua kuwa hawana ubavu wa kufanya maandamano na mikutano nchi nzima Septemba 1 na kwamba walichofanya ni kuwatia hofu wananchi.

“UVCCM tulijua, tulielewa na kutambua bayana kwamba Chadema walikuwa wanafanya maigizo katika siasa, hawana ubavu wala jeuri ya kuandamana kwa madai ya kipuuzi na ambayo sio ya msingi kwa mustakabali wa nchi yetu,” alisema Shaka.

Aidha, Shaka alikanusha sababu zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kuahirisha maandamano hayo kuwa wameombwa na viongozi wa dini ili waweze kukaa na pande zote kujaribu kutafuta suluhu kwa amani.

“UVCCM inatamka bayana kuwa hakuna majadiliano, mazungumzo wala mijadala itakayojadiliwa kati ya Serikali ya CCM na Chadema. Tunaomba Serikali ya Rais John Magufuli iendelee na mikakati yake ya kisera,” Shaka ameongeza.

Kaimu Katibu Mkuu huyo wa UVCCM alisisitiza kuwa Chadema hawana ubavu wa kufanya maandamano na mikuano nchi nzima Oktoba 1 kama walivyosema, baada ya kushindwa kufanya hivyo Septemba 1.

Shaka amesema wanachokifanya hivi sasa Chadema kinatokana na kushindwa kubuni mikakati ya kufanya siasa ili chama chao kiimarike na kukubarika.

Jana, Chadema walitangaza kuahirisha uzinduzi wa oparesheni UKUTA nchi nzima, iliyokuwa imepangwa kufanyika leo (Septemba 1) kwa maandamano na mikutano nchi nzima.

UVCCM pia walitangaza kuahirisha maandamano yao ya nchi nzima waliyokuwa wamepanga kuyafanya Agosti 31 kwa lengo la kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi aliyoifanya ndani ya kipindi kifupi.

Maandamano ya pande zote mbili yalipigwa marufuku na Jeshi la Polisi nchini.

Henrikh Mkhitaryan Yu Shakani Kuwakabili Man City
Mapokezi ya Waziri Mkuu Mjini Dodoma leo Yaahirishwa