Ripoti mpya na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya madawa na uhalifu – UNDOC, kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu inaelezea hofu kwamba rasilimali za kuwaokoa waathirika wa usafirishaji huo, zimeelekezwa kwenye janga la Uviko-19.
Takwimu za UNODC, zinaonyesha kwamba waathirika walioweza kutoroka wamefanya hivyo bila msaada wowote na hofu ni kwamba janga wa Uviko-19 limezilazimisha serikali kuelekeza rasilimali za shughuli za polisi kukabiliana na uhalifu huo ikiwemo mitandao ya wasafirishaji haramu.
Kwa mujibu wa UNODC, matokeo ya utafiti wa ripoti hiyo yanajumuisha tathimini ya kesi 800 zilizo mahakamani na mapendekezo ya kina kwa watunga sera, ili kusaidia kuweka mikakati Madhubuti ya hatua kwani janga la Uviko-19 linaendelea kuweka mazingira mabaya na kudhoofisha uwezo wa kuokoa waathirika na kuwafikisha wahalifu kwenye mkono wa sheria.
Pia ripoti hiyo, imebaini kwamba idadi ya waathirika wa usafirishaji haramu kote duniani ilipungua kwa asilimia 11% na idadi ya hukumu zilizotolewa kutokana na makosa ya usafirishaji haramu wa binadamu pia zilipungua kwa asilimia 27 mwaka 2020, huku ripoti ikionya masharti wakati wa janga la COVID-19 huenda yaliisukuma baadhi ya mifumo ya usafirishaji haramu wa binadamu kuingia katika maeneo yaliyojificha zaidi.
Ripoti inasema kupungua kwa kiasi kikubwa kwa hukumu za makosa ya usafirishaji haramu wa binadamu kumeripotiwa Asia Kusini kwa asilimia 56%, Amerika ya Kati na Caribbea asilimia 54 na Amerika Kusini asilimia 46.