Maafisa, Wakaguzi na Askari wa Jeshi la Polisi Wilayani Handeni mkoani Tanga Disemba 13, 2023 wametakiwa kutumia hekima wakati wa kutekeleza majukumu yao, ili kuhakikisha haki inatendeka.
Kamanda wa Polisi mkoa Tanga ACP, Almachius Mchunguzi ametoa kauli hiyo wakati akiendelea na zoezi la ukaguzi Wilayani Handeni na kusema kufuata sheria, nidhamu na kutumia hekima ndiyo msingi unaowezesha kutenda haki kwa watendaji hao wakati wa kutimiza majukumu yao ya kila siku.
Amesema kupitia ukaguzi huo (Formal Inspection) wa robo tatu ya mwaka amelenga kuongeza morali na kutoa motisha kwa askari ili waweze kufanya vizuri na kubainisha kuwa kwa sasa Jeshi la Polisi linatekeleza majukumu yake kwa weledi na kufuata sheria ikiwemo kufuata muongozo wa utendaji wa Jeshi la Polisi (PGO).
Aidha, Kamanda Mchunguzi amewataka Maafisa, Wakaguzi na Askari kuimarisha utendaji wao huku akihimiza hekima na busara kuongoza utendaji wa askari hao, huku akitumia jukwaa hilo kuwaasa Maafisa, Wakaguzi na Askari kushirikiana katika mambo mbalimbali ya kijamii na kimaendeleo ili kufikia malengo yao.