Shirikisho la soka nchini Tanzania ‘TFF’ limeutaka Uongozi wa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kufanya maboresho katika eneo la kuchezea na maeneo mengine Uwanjani hapo, ili kufikia viwango vya ubora wa Kimataifa.

Uwanja wa CCM Kirumba kwa muda mrefu umekua hautumiki kwa michezo ya Kimataifa upande wa Vilabu au Timu ya Taifa, kutokana na kukosa vigezo maalum vilivyoweka na Shirikisho la soka Barani Afrika ‘CAF’ pamoja na ‘FIFA’.

Katibu Mkuu wa TFF Wilfred Kidao mapema leo Jumanne (April 25) amekutana na Uongozi wa Uwanja huo na kutoa maelekezo hayo, huku akiahidi kupelekwa kwa michezo ya Kimataifa Uwanjani hapo, endapo vigezo vitatimizwa kwa baadhi ya maeneo kufanyiwa marekebisho.

Kidao amesema Uwanja wa CCM Kirumba umekua na sifa zote za kuhodhi michezo ya kimataifa, lakini unakwamishwa na baadhi ya maeneo kukosa sifa zinazotakiwa na CAF pamoja na FIFA.

“Nimekutana na Meneja wa Uwanja na tumekubaliana kuwa, ni lazima baadhi ya maeneo ya uwanja huu yafanyiwe maboresho ili kurejesha hadhi ya kuchezwa kwa michezo mikubwa ya kimataifa upande wa Timu ya Taifa na Vilabu.”

“Umekua na michuano mingi ya kimataifa, lakini kwa kipindi kirefu Uwanja wa CCM Kirumba hautumiki kwa sababu sifa zake hazikidhi vigezo vilivyowekwa, nimemwambia meneja kwa kushirikiana na wamiliki wa Uwanja huu wayafanyie kazi mapungufu yaliopo, halafu tutaangalia namna ya kuanza kuutumia kwa michezo ya kimataifa.”

“Niaamini kama niliyoshauri yatafanyiwa kazi, mashabiki wa hapa Mwanza na Kanda ya Ziwa watakuwa na nafasi nyingine ya kushuhudia michezo ya kimataifa ikichezwa hapa na pia watawaona wachezaji wakubwa wakija hapa kupambana.” amesema Kidao.

Mara ya mwisho Uwanja wa CCM Kirumba ulikua mwenyeji wa Mchezo wa Kimataifa upande wa vilabu kati ya Young Africans na Pyramid FC ya Misri kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika misimu mitatu iliyopita.

Bikira wa miaka 70 adai ufupi ndio chanzo cha kukosa mume
Nabi afichua siri ya kuibamiza Simba SC Jumamosi