Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetangaza kuandaa mchakato wa kuujenga upya Uwanja wa CCM Mkwakwani uliopo jijini, Tanga ili kufikia vigezo vya kimataifa, imeelezwa.
Rais wa TFF, Wallace Karia, alisema hayo mwishoni mwa juma lililopita wakati akizungumza na wadau wa soka wa mkoa wa Tanga akiwamo Mkurugenzi wa Hoteli ya Tanga Beach Resort, Hamisi Kindoroko na Katibu wa CCM (Muheza), Mohamed Moyo.
Karia alisema tayari ameshazungumza na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella na wadau wengine ili kuanza maandalizi ya ukarabati wa uwanja huo ambao utasaidia kuinua kiwango cha wachezaji wa jijini hapa.
Alisema sasa hivi wanatarajia kufanya mazungumzo na uongozi wa CCM Mkoa wa Tanga ili kupata ridhaa ya kuanza mchakato huo kwa sababu wao ndio wamiliki wa uwanja.
Tunataka kuona uwanja wa Mkwakwani unakarabatiwa na kuwa wa kisasa kabisa ili mechi za kimataifa ziweze kuchezwa katika uwanja huo wa siku nyingi, kama mnavyojua Tanga ni waja leo waondoka leo,” alisema Karia.
Katibu wa CCM (Muheza), Mohamed Moyo, alisema wanamshukuru Karia kwa maandalizi yake ya kujenga upya uwanja wa Mkwakwani na kumwomba pia kuutizama na Uwanja wa Jitegemee ambao pia unahitaji matengenezo.
Chanzo: Gazeti la Nipashe