Ukuta wa uwanja wa mpira wa miguu jijini Dakar nchini Senegal umebomoka na kuua watu wanane huku watu 90 wakijeruhiwa, baada ya mashabiki wa timu mbili hasimu za Stade de Mbour na Union Sportive Ouakam  kufanya vurugu katika fainali ya ligi ya nchi hiyo.

Tukio hilo lilitokea jana baada ya jeshi la polisi nchini humo kujaribu  kutuliza vurugu hizo kwa kufyatua mabomu ya machozi kati ya mashabiki wa timu hizo ambao walikuwa wakirushiana vitu ikiwa ni pamoja na mawe, muda mfupi baada mpira kumalizika.

Kuporomoka kwa ukuta wa uwanja huo kulitokana na idadi kubwa ya mashabiki kujaribu kuondoka uwanjani hapo kwa kuruka sehemu moja ya ukuta, hali iliyopelekea kulemewa na kuanguka.

Dakika 90 za mpira huo zilimazika kwa sare ya 1-1, lakini baada ya kuongeza dakika timu ya Mbour ilifanikiwa kutikisa nyavu tena na kuyafanya matokeo kuwa 2-1  na vurugu zilianza punde tu baada ya muamuzi kupuliza kipyenga cha mwisho.

“Ghafla tu wakati ukuta unaanguka… nilijua tayari kuna wenzetu wamepoteza maisha kwa sababu ukuta ulianguka moja kwa moja kuelekea watu walipokuwa,” Cheikh Maba Diop, shuhuda wa tukio hilo aliiambia shirika la habari la AFP.

Kutokana na tukio hilo, Serikali ya nchi hiyo imepiga marufuku kufanyika kwa shughuli zote za michezo na utamaduni kwa kipindi cha mwezi mmoja.

Msemaji wa Rais Macky Sall amesema kuwa kutokana na tukio hilo baya, mchakato wa kampeni za uchaguzi ujao umeahirishwa kwa lengo la kuonesha heshima na kwamba adhabu kali itatolewa kama sehemu ya fundisho na onyo kwa vitendo kama hivyo.

Serikali ya Senegal pia imetangaza kufanya uchunguzi haraka kuhusu tukio hilo na kuchukua hatua stahiki.

Hata hivyo, kumekuwa na maoni kuwa sehemu ya ukuta wa uwanja huo haikuwa na uimara wa kutosha.

Korea Kusini yataka yafanyike mazungumzo na Korea Kaskazini
Magazeti ya Tanzania leo Julai 17, 2017