Uwanja wa Namfua unaomilikiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ulioko mkoani Singida unaendelea kukarabatiwa kupata hadhi ya timu kubwa kutimua vumbi kwenye msimu ujao wa Ligi Kuu, huku klabu ya Singida United ikiwa mwenyeji.
Kwa mujibu wa uongozi wa uwanja huo, hatua za awali za ukarabati ambazo ni pamoja na usawazishwaji zimekamilika na hivi sasa wanajaza udongo kwa ajili ya kuanza kuotesha nyasi.
Uwanja huo unatarajiwa kuanza kutumika rasmi Agosti mwaka huu ambapo mechi zote za nyumbani (mkoani Singida) zitashuhudiwa katika uwanja huo.
Timu ya Singida United itaanza kuutumia uwanja huo baada ya marekebisho, ikiwa na baraka za kuwa chini ya kocha mpya mholanzi, Hans Pluijm aliyewasajili wachezaji watatu wa kigeni. Timu hiyo ni miongoni mwa timu tatu zilizopanda daraja na kupata sifa za kushiriki msimu ujao wa Ligi Kuu.
Timu nyingine zilizopanda daraja ni Njombe na Lipuli FC.