Serikali imesema inatarajia kutumia kiasi cha Shilingi Bilioni 35 kuboresha uwanja wa ndege wa Musoma, mkoani Mara, kwa kuweka lami na kuongeza urefu wa uwanja huo ili kuruhusu ndege kubwa na ndogo kuweza kutua.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho, alipofika uwanjani hapo kukagua maandalizi ya ujenzi huo.
Aidha, Waziri Chamuriho, ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa huo na vitongoji vyake ambao watapata ajira katika mradi huo, kuhakikisha kuwa wanatumia vizuri fursa watakayoipata kwa kuwa waaminifu na kufanya kazi kwa bidii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt. Khalfani Haule, amesema kuwa mradi huo ukikamilika utarahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kwa wananchi wa Musoma na pia kuchochea biashara ya utalii kupitia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo ipo mkoani humo.
Ameongeza kuwa Uongozi wa Wilaya tayari umejipanga kwa kuupokea mradi huo na wameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Mkandarasi huyo kwa kumpatia eneo la kuchimba mchanga na kokoto za ujenzi.
Naye, Meneja wa Uwanja wa ndege wa Musoma, Mohammed Bakari, amesema kuwa, uwanja huo utajengwa na Kampuni ya kikandarasi ya Beijing kutoka China ambapo itatumia miezi 20 kuanzia mwezi Aprili, 2021 na kutarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2022.
Amefafanua kuwa Mkandarasi huyo tayari ameshawasilisha vifaa vyake katika eneo la mradi kwa ajili ya kuanza rasmi ujenzi huo, na kusisitiza kuwa ujenzi wa uwanja huo unasimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Mara.