Viongozi wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT) Wilaya ya Njombe mkoani Njombe, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya wilaya hiyo, Anjela Mwangeni wamefanya ziara ya Kikazi katika Matawi ya Kihesa, Mgendela, Idundilanga na Kambarage Kata ya Njombe mjini kwa lengo la kuzungumza na wanachama.
Akizungumza na Wanachama katika Matawi hayo Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Njombe, Anjela Mwangeni amewataka wanawake wilayani humo kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali Serikalini pindi uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakapoanza, ili waweze kuitetea nafasi ya Mwanamke katika Jamii.
“Akina mama tuna nafasi kubwa katika Jamii, naomba tujitokeze kwa wingi katika kuomba na Kugombea nafasi mbalimbali Serikalini kwenye uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa ili tuweze kuwatetea Wanawake wenzetu, pia naomba tuendelee kukiamini chama cha mapinduzi kinachoongoza Serikali yetu,”amesema Mwangeni
Kwa upande wake Katibu wa UWT Wilaya ya Njombe, Nuru Mwaibako ametoa wito kwa Viongozi wa Jumuiya hiyo kuhakikisha wanakutana Kikatiba na kufanya Vikao vya kiutendaji kisha kutoa elimu kwa Wanachama ili kuendelea Kuimarisha Jumuiya na kukijenga chama cha mapinduzi.