Johansen Buberwa – Kagera.
Mkandarasi wa Kampuni ya EFQ Limited, anayetekeleza mradi wa Maji wa Kashenye, Mugana na Kanyigo awamu ya kwanza kusimamiwa na RUWASA katika Wilaya Misenyi Mkoani Kagera, ametakiwa kukamilisha kazi kwa wakati, ili Wananchi waweze kuondokana na adha ya maji na kumtua Mama ndoo kichwani.
Wito huo, umetolewa na Mjumbe wa utekelezaji wa Umoja wa Wanawake – UWT, Taifa na Katibu wa Bunge wa Kamati ya Fedha ya Bajeti, Subira Mgalu baada ya kukagua mradi huo, Tanki la lita 200,000, vibanda 10 vya huduma ya maji, ujenzi wa mitaro ya kulaza mabomba ya urefu wa kilomita 14.3 utakaowanufaisha wananchi zaidi ya 16,000 ndani ya kata tatu na unaogharimu zaidi ya shilingi Bilioni 1.867.
Amesema, Mradi huo unaotekelezwa kwa muda wa miezi sita ambapo wananchi wake walikuwa kitembea umbali mrefu kwa zaidi ya masaa matano utamsaidia kila mwananchi kufikiwa na huduma Maji na kumtaka Mkandarasi anayesimamia mradi huo ulioanza Mei 25, 2023 kukamilisha kazi kazi hiyo Novemba 25, 2023.
Awali, Mjumbe wa UWT Taifa Uchumi na Mipango, Regina Zachwa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajiri ya maendeleo yanayoendelea kupatikana ndani ya mkoa huo hali inayoendelea kuleta matumani kwa wananchi kwani Mkoa huo unazidi kunufaika na miradi mbalimbali ya kimaendeleo.
Kwa upande wao baadhi ya Wananchi wa kata hizo akiwemo Theresia Gasper amesema wamekuwa wakihangaika na Watoto kutafuta maji hivyo kukamilika kwa mradi huo kutawaokoa na adha waliyokuwa wakiipata awali.