Serikali kupitia Wizara ya Afya imekabidhi mashine tano za kisasa za kuchanganya chumvi na madini joto kwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI zilizotolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kupitia shirika la Kimataifa la Nutrition Intenational kwa ajili ya kusimikwa katika Mikoa ya Tanga, Pwani na Mtwara ili kusaidia kuongeza uzalishaji wa chumvi yenye kiwango cha kutosha cha madini joto nchini.
Akikabidhi mashine hizo leo Februari 24,2022 jijini Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema Utafiti uliofanyika nchini mwaka 2019 ulibaini Tanzania inazalisha chumvi Tani 330,712 kwa mwaka na kati ya Chumvi hiyo Tani 141, 22 ambapo ni sawa na asilimia 43 haiwekwi madini joto hivyo ujio wa mashine hizo utasaidia kuongeza uzalishaji wa chumvi yenye madini hayo.
Prof Makubi amesema mashine hizo ambazo zimetengenezwa nchini na wataalamu kutoka VETA zimeweza kugharimu kiasi cha shilingi milioni 55 huku gharama ya mashine moja ikigharamu kiasi cha shilingi milioni 11 na kusaidia kuokoa milioni 14 kwa kila mashine endapo zingeagizwa kutoka nje ya nchi.
“Mwaka 2018 shirika la Nutrition International ilifadhili ununuzi wa mashine tatu zilizoagizwa kutoka Afrika Kusini kwa jumla ya Shilingi milioni 75 ambapo mashine moja iligharimu shilingi Milioni 25 na kusimikwa Halmashauri za Kilwa, Hanang na Meatu na zinaendelea kufanya kazi na safari hii mashine hizo zimeweza kutengenezwa na Watalaam wetu kutoka VETA kusaidia kuokoa shilingi milioni 14 kwa kila mashine” amesema Prof Makubi.
Hata hivyo Prof.Makubi amezitaka Halmashauri zinazozalisha chumvi kusimamia kikamilifu wazalishaji kuchanganya chumvi na madini joto ili kuondokana na madhara hayo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Prof.Riziki Shemdoe, amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa iliyopatiwa mashine hizo kuhakikisha zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na sio kuzifungia.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Caroline Nombo, amesema kuwa kutokana na maboresho ya mafunzo na ufundi stadi nchini, VETA imetengeneza mashine hizo na kuokoa fedha za serikali ambazo zingetumika kununua nje ya nchi.