Hatimaye Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, wakishirikiana na Mzabuni wa ubunifu na mauzo ya Jezi za msimu mpya 2021/22, wametangaza Septemba 04, kuwa siku maalum ya uzinduzi wa Jezi mpya za klabu hiyo.
Kaimu Afisa Habari wa Simba SC Ezekiel Kamwaga, ameongoza mkutano na waandizhi wa habari uliofanyika leo mchana jijini Dar es salaam katika hoteli ya Hyatt Regency, ambapo amesema uzinduzi wa jezi mpya wa klabu hiyo ni sehemu ya safari ya kuelekea kwenye Tamasha la Simba Day litakalofanyika Septemba 19, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
“Tuko hapa kuzungumza kuhusu jezi zetu mpya ambazo zitatolewa na mzabuni wetu mpya kampuni ya Vunja Bei.”amesema Ezekiel Kamwaga
Naye Mkurugenzi Kampuni ya Vunja Bei ambayo ndio Mzabuni wa ubunifu na mauzo ya Jezi mpya za Simba SC, Fred Vunja Bei amesema: “Uzinduzi wa jezi za Simba tutafanya Jumamosi Septemba 4, 2021 saa 1:00 usiku kwenye hoteli ya Hyatt Regency. Litakuwa tukio ambalo litahusisha wadau mbalimbali, pia tutakuwa live kupitia Azam TV.”
“Jambo moja naweza kusema ni jezi nzuri sana. Tutakuwa na jezi za aina tofauti sana ukilinganisha na timu zingine za ndani. Baada ya uzinduzi jezi zitakuwepo kwenye maduka ya Vunja Bei na tutauza masaa 24.” Amesema Fred Vunja Bei