Ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Wolfsburg, umempa nafasi meneja wa klabu ya Man Utd, Louis van Gaal kuwaomba wachezaji wake kutobweteka na matokeo hayo, na badala yake wafanye kazi ya ziada kama kweli wanahitaji kusonga mbele kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu huu.
Van Gaal, ametoa rai hiyo kwa wachezaji wake mara baada ya mchezo huo ambao uliunguruma kwenye uwanja wa Old Trafford ambapo kila shabiki wa Man Utd alihitaji mambo kuwa mazuri usiku wa kuamkia hii leo.
Van Gaal, amesema michuano ya msimu huu ina changamoto kubwa na hakuna njia ya mkato kwa wachezjai wake ambayo wanapaswa kupita zaidi ya kupambana wakati wote na kuamini hakuna mwenye uwezo mdogo.
Amesema ilikua ni vigumu kwa wachezaji wake kuvuna ushindi wa mabao mawili kwa moja kutoka kwa Wolfsburg, waliofunga safari wakitokea nchini Ujerumani kutokana na upinzani mkali uliokuwepo, lakini ujasiri na uvumilivu wa kikosi chake ulikua chachu ya kupatikana na mazuri yaliyoonekana baada ya dakika 90.
Katika mchezo huo Man utd walitanguliwa kufungwa bao na Wolfsburg, katika dakika ya 4 kupitia kwa kiungo kutoka nchini Ujerumani Daniel Caligiuri, lakini dakika 30 baadae kiungo kutoka nchini Hispania Juan Mata alisawazisha kwa njia ya mkwaju wa penati kabla ya Chris Smalling hajafunga bao la pili katika dakika ya 54.
Kama itakumbukwa vyema Man Utd walipoteza mchezo wa mzunguuko wa kwanza wa hatua ya makundi wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kwa kukubali kufungwa mabao mawili kwa moja dhidi ya mabingwa wa soka kutoka nchini Uholanzi PSV Eindhoven.
Matokeo ya michezo mingine ya ligi ya mabingwa barani Ulaya hatua ya makundi iliyochezwa usiku wa kuamkia hii leo.
Champions League – Group A
Malmoe FF 0 – 2 Real Madrid
Shakhtar Donetsk 0 – 3 Paris Saint Germain
Champions League – Group B
CSKA Moscow 3 – 2 PSV Eindhoven
Manchester United 2 – 1 Wolfsburg
Champions League – Group C
Astana 2 – 2 Galatasaray
Atletico Madrid 1 – 2 Benfica
Champions League – Group D
Borussia Moenchengladbach 1 – 2 Manchester City
Juventus 2 – 0 Sevilla