Baada ya kuwasili Dar es salaam na kupokelewa kwa shangwe na Mashabiki Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck, amesema leo Ijumaa anaanza kupanga mikakati ya kuikabili Young Africans kwenye mchezo Nusu Fainali Kombe La Shirikisho (ASFC) utakaochezwa Jumapili.
Kocha Sven, amesema hakutaka kuufikiria mchezo huo mapema kwa sababu anaifahamu vyema Young Africans hivyo, safari hii wasubiri kuona makali na hasira za kikosi chake.
Amesema hata walipokuwa wakiwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baadhi ya wapinzani wao walikisema kikosi chake lakini mwisho wake wameshuhudia kombe likitua Msimbazi kwa msimu wa tatu mfululizo.
Kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji amesema mchezo huo kwake ni rahisi kwa sababu amebakiza “hesabu” za kuwania taji hilo bila ya presha ya kuwaza tiketi ya kushiriki michuano ya kimataifa kama walivyo watani zao Young Africans.
“Sikuwahi kuifikiria Yanga kabla ya kumaliza michezo ya ligi iliyokua inatukabili Mtwara na Lindi, sasa ndio ninaanza mikakati ya kuelekea mchezo huo wa Nusu Fainali, tuna siku mbili za mazoezi, zinatosha kuimarisha mipango yetu,” alisema Sven.
Kocha huyo amesema atakuwa na uhuru wa kupanga kikosi chochote baada ya baadhi ya nyota wake kupumzika katika mchezo uliopita dhidi ya Namungo FC ambao ulimalizika kwa suluhu.
“Sitaki kuwaahidi mashabiki nini tutafanya, hii imebaki baina yangu na wachezaji, nitazungumza na kuwaambia wanachotakiwa kukifanya Jumapili, tusubiri,” Mbelgiji huyo aliongeza.
Simba SC walitinga hatua ya Nusu Fainali Kombe La Shirikisho (ASFC) baada ya kuifunga Azam FC Mabao mawili kwa sifuri, huku Young Africans wakiivurumisha Kagera Sugar mabao mawili kwa moja.