Kocha mkuu wa klabu bingwa Tanzania Bara Wekundu wa Msimbazi Simba Sven Vandenbroeck, amewapongeza Young Africans kwa kufanya usajili mzuri kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu, ambao utaanza mwishoni mwa juma hili kwenye viwanja tofauti.

Kocha Sven, ametoa pongezi hizo wakati kikosi chake kikiwa safari kuelekea jijini Mbeya kupitia Dares salaam, tayari kwa mchezo wa ufunguzi wa msimu wa 2020/21 dhidi ya Ihefu FC, utakaochezwa mwishoni mwa juma hii.

Simba ilikua jijini Arusha ambako ilicheza mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Namungo FC ambao walikubali kufungwa mabao mawili kwa moja siku ya Jumapili, na jana Jumatatu ilicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya AFC inayoshiriki Ligi Daraja la kwanza, na kuibuka na ushindi wa mabao sita kwa sifuri.

Kocha huyo kutoka nchini Ubelgiji amesema, msimu huu anatarajia upinzani mkali kutoka kwenye klabu zote za Ligi Kuu, kutokana na usajili mzuri uliofanywa, hasa kwa washindani wake Young Africans ambao walimaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo msimu uliopita.

“Ligi itakuwa ngumu kwa kuwa timu zinaonekana kujiandaa vizuri hususan katika usajili. Yanga imefanya usajili mzuri, kutakuwa na changamoto kubwa ya ubingwa”.

Young Africans mwishoni mwa juma lililopita iliwatambulisha wachezaji waliowasajiliwa kwa ajili ya msimu wa 2020/21, kwenye Tamasha la SIKU YA MWANANCHI lililofanyiwa Uwanja wa Mkapa, Dar es salaam.

Wachezaji waliosajiliwa na klabu hiyo Makipa ni Farouk Shikalo, Metacha Mnata na Ramadhan Kabwili

Mabeki

Paul Godfrey, Kibwana Shomari, Yassin Mustafa, Adeyum Saleh, Lamine Moro, Said Makapu, Bakari Nondo Mwamnyeto na Abdallah Shaibu Ninja.

Viungo.

 Zawadi Mauya, Feisal Toto, Haruna Niyonzima, Abdulaziz Makame, Mukoko Tonomb, Balama Mapinduzi, Deus Kaseke, Juma Mahadhi, Farid Mussa,Tuisila Kisinda na Carlos Carlinhos.

Washambuliaji.

Wazir Junior, Ditram Nçhimbi, Yacouba Songne, Michael Sarpong na Adam Kiombo.

Kwa upande wa Ligi Kuu, ambayo itaanza mwishoni mwa juma hili Simba itakuwa ugenini kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa kuivaa Ihefu FC, wakati Namungo ikianzia nyumbani kwenye Uwanja wa Majaliwa ikiwakaribisha Coastal Union, huku Young Africans ikiwa mwenyeji wa Tanzania Prisons katika Uwanja wa Mkapa.

Chato - Nyabilezi, Igando yanufaika kwa mawasiliano
Neema yavishukia vyuo vya kilimo nchini